Kwanini taratibu za udhibiti wa mazingira (EMS) ni muhimu kwa mashirika yasiyo ya kiserikali?
EMS huweza kuwa chombo cha maendeleo ya kiuchumi na utunzaji wa mazingira, hasa wakati hujumuisha umma katika utendaji wake. EMS ni muhimu hasa kwa nchi zinazoendelea kwa kuwa hufanikisha ugawanyaji wa mali ghafi adimu na hutafuta njia zisizo za gharama za kupunguza utoaji wa hewa chafu na uharibifu wa mazingira. Viwanda na kampuni zisizo na bajeti kwa ajili ya ununuzi wa teknolojia za kupunguza uharibifu wa mazingira huweza kuanza kupunguza uharibifu huo kwa kuwa na taratibu nzuri zinazodhibiti utengenezaji wa bidhaa ili kupunguza utumizi mbovu wa mali ghafi. Taratibu hizi huweza pia kuongeza utendaji katika kiwanda au kampuni na huweza kuongeza mapato ya uzalishaji.

Kwa nini ni muhimu kuhusisha umma na kuwa na utangazaji kuhusu utendaji wa EMS?
Utangazaji wa utendaji katika udhibiti na utunzaji wa mazingira huongeza uwezekano kuwa EMS italeta mafanikio ya kweli. Kwa sasa hivi, ISO 14000 inaruhusu kampuni na viwanda kuweka malengo kuhusu upunguzaji wa utoaji wa hewa chafu au uharibifu wa mazingira, lakini haihitaji kampuni kutangaza ufanikishaji wa malengo haya. Mashirika yasiyo ya kiserikali na umma kwa ujumla huweza kudhibit utendaji wa kampuni kwa kuhitaji kampuni na viwanda kutangaza utendaji wao wakifuata taratibu za ISO 14001 (ISO 14001 ni kitengo cha ISO 14000 kinachotoa maongozo kuhusu udhibiti wa mazingira).

NGOs zinawezaje kuhakikisha kuwa EMS huhusisha umma?
NGOs au mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kusaidia viwanda na kampuni kuhusisha umma katika utendaji wa EMS kwa kuhakikisha kuwa viwanda na kampuni hutangaza mara kwa mara utekelezaji wa taratibu za ISO. Mashirika yasiyo ya kiserikali ni lazima yajielimishe zaidi kuhusu utumikaji wa ISO 14001 na yajulishe uongozi wa ISO 14000 kuhusu ukosefu wa uhusishaji wa umma katika utekelezaji wa taratibu za ISO 14001. (Maelezo kuhusu uongozi na taratibu za ISO 14000 hupatikana katika mtandao ufuatao: http://www.tc207.org/aboutTC207/index.html).

Mashirika yasiyo ya kiserikali ni lazima pia yajielimishe kuhusu taratibu za ISO 14000 - jinsi zinatayarishwa, jinsi zinatumika na sehemu zinazotumika. Mtandao wa ECOLOGIA http://www.ecologia.org/ems/iso14000/ hutoa maelezo zaidi kuhusu ISO 14000. Jumuiya ya kimataifa ya taratibu za utengenezaji wa bidhaa (ISO) pia hutoa maelezo katika mtandao wake: http://www.tc207.org/.

Mashirika yasiyo ya kiserikali au NGOs huwezaje kuchangia katika upanuzi wa EMS?
Mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kuelimisha kuhusu EMS na taratibu za ISO hasa kwa viwanda na kampuni ndogo ndogo. Washauri wakulipwa huweza kushauri kampuni kununua shahada za ISO 14000 kwa bei kubwa bila kuhimiza udhibiti wa mazingira. Mashirika yasiyo ya kiserikali huweza kuwa chanzo cha maelezo kuhusu taratibu za udhibiti wa mazingira au EMS.

NGOs zinaweza kuchangia katika utayarishaji wa taratibu za ISO?
Ndiyo. NGOs zinaweza kuongeza uhusishaji wa umma kwa kujihusisha na utayarishaji wa taratibu za ISO. Kwa sasa hivi, kamati inayoangalia utayarishaji wa taratibu hizi inawawakilishwa na viwanda vikubwa. Kamati hii ina wawakilishi wachache kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali na kutoka umma kwa ujumla. Kuna umuhimu wa kujumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali na yasiyo ya kibiashara katika utayarishaji wa taratibu za ISO 14000. Ni muhimu kupata maelezo kutoka kamati ya ISO 14000 ya nchi yako kuhusu malengo ya kuhusisha mashirika yasiyo ya kiserikali na kibiashara katika utayarishaji wa taratibu hizi.

NGOS zinawezaje kuchangia katika utekelezaji wa taratibu za ISO?
NGOs zinaweza kuangalia kuwa kampuni na viwanda vinatekeleza taratibu zilizowekwa na ISO za udhibiti wa mazingira kwa kujihusisha na usimamizi wa utekelezaji wa taratibu hizi. NGOs zinaweza kushauri kampuni na viwanda katika ufanikishaji wa malengo ya udhibitia na utunzaji wa mazingira ili utendaji uwe wa kiwango zaidi ya kile kilichowekwa na ISO.

This fact sheet was written and translated for ECOLOGIA by Middlebury College student Laura Tarimo. August, 2002.